JENGO LA MAMA NA MTOTO LAWEKEWA JIWE LA MSINGI

Posted on: September 12th, 2019

Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein,  Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi   aliwakilishwa na Dr. Sila (Mb) Waziri wa Ujenzi Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka jiwe la msingi katika jengo la Mama na Mtoto la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou – Toure tarehe 08-12-2019.  Akitoa salamu kwa wananchi wa mkoa wa mwanza waliohudhuria sherehe hiyo kutoka kwa Mh. Rais wa Zanzibar alisema kuwa  awamu hii ya tano ni awamu ambayo ina malengo ya kuleta mabadiliko katika sekta ya afya pamoja na sekta zingine. Alisema kuwa anaona fahari kubwa kuona mabadiliko ambayo yanazidi kutekelezeka na ndio maana tunaona ujenzi wa jengo la mama na mtoto ambao unaendelea alitaja miradi katika hospitali ambayo imeishatekelezwa kama ujenzi wa tanki la maji, jengo la Bima ya Afya, jengo la kusubiria wagonjwa na ujenzi wa vyoo vya kisasa vya wagonjwa.  Vile vile alisema kuwa jengo hilo  lililoanzwa kujengwa tangu tarehe 01.10.2017 na linategemewa kumalizika 01.06.2020. 

Akitoa salamu   Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo hilo lililopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure alisema utoaji wa huduma za Afya  katika hospitali ya Sekou Toure umeendelea kuimarika katika maeneo mbali mbali, kwa upande wa dawa, vifaa na vifaa tiba, serikali ya awamu ya tano imeongeza bajeti kutoka kiasi cha shilingi milioni 147 kwa mwaka 2014/2015 hadi kufikia milioni 407 kwa mwaka 2018/2019 na hii imefanikisha uhakika na upatikanaji wa dawa muhimu (tracer medicine) kwa asilimia tisini nne (94%).


Kwa upande wa watumishi kumekuwepo na ongezeko la watumishi wa kada mbali mbali: Madaktari Bingwa kutoka watatu (3) waliokuwepo mwaka 2015 na kufikia Madaktari Bingwa kumi na mmoja (11) mwaka 2019. Wizara pia imeendelea kuhakikisha kuwa inasomesha na kuajiri watumishi wa kada nyingine hasa za udaktari, uuguzi na Wateknolojia.

Kutokana na mafanikio hayo, idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika hospitali imeongezeka kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku katika mwaka 2015 na kufikia wastani wa wagonjwa kati ya 500 hadi 700 kwa siku kwa  mwaka 2019.


Jengo hilo lina ghorofa sita (G+5) lenye ukubwa wa mita za mraba 10,918 litakalokuwa na uwezo wa vitanda 230 na kuweza kutoa huduma zote za afya ya uzazi , huduma za magonjwa ya akina mama pamoja na watoto. Mradi huu unatarajiwa kugharamia jumla ya shilingi Bilioni 10,106,468,902.31 mpaka kukamilika kwake bila vifaa tiba. Mradi huu unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.