FAHAMU KUHUSU UGONJWA WA UVIKO 19 (COVID 19)

Posted on: August 20th, 2022

Mnamo Januari 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa ugonjwa mpya wa virusi vya korona katika Mkoa wa Hubei, Uchina, kuwa suala la Hali ya Hatari ya Afya ya Umma Kimataifa kwa sababu ya uwezekano mkubwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona vya mwaka 2019 (UVIKO-19) kuenea duniani kote. Kufikia Aprili 2 2020, wagonjwa zaidi ya 896, 450 wameambukizwa katika nchi zaidi ya 200, zaidi ya watu 45, 526 wamekufa kutokana na ugonjwa huo, lakini wengine 135,000 pia wametibiwa na kupona tangu kuzuka kwa ugonjwa huo. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki matukio ya ugonjwa huu wameripotiwa nchini Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania. Watu wengi walioambukizwa huonyesha dalili zisizo kali na kiwango cha takribani 4% cha vifo ulimwenguni ni cha chini kikilinganishwa na magonjwa mengine ya kuambukiza yanayotokea ukanda huu kama vile VVU/UKIMWI, surua au Ebola. Janga hili  halijaathiri tu sekta ya afya, bali limeathiri uchumi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na biashara na utalii, ambazo ndio nguzo kuu za maisha katika ukanda huu.

Ili kufanikiwa katika kukabiliana na janga hili, makundi yote katika jamii yetu ikiwa ni pamoja na waajiri na wafanyabiashara – ni lazima yahusike na kushirikiana. Kirusi ambacho husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ni cha aina mpya ambacho hakikuwa kimewahi kutokea kwa binadamu hadi ugonjwa huo ulipozuka mwaka wa 2019.

Virusi vya Korona (ViKo) ni kundi kubwa la virusi ambavyo kwa kawaida hupatikana kwa wanyama na husababisha maradhi hatari yanyohusiana na upumuaji kama vile Dalili za Upumuaji za Middle East (Middle East Respiratory Syndrome (MERS-CoV) na Dalili Kali na Hatari za Upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS- CoV).

Virusi vya korona huambukizwa baina ya wanyama na watu. Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa virusi vikali na hatari vya SARS-CoV viliambukizwa binadamu kutoka paka aina ya ngawa navyo virusi vya upumuaji vya MERS-CoV viliambukizwa binadamu kutoka ngamia wenye nundu moja. Kuna virusi vya korona vingine vinavyojulikana kuwa vinapatikana miongoni mwa wanyama bila kusababisha ugonjwa kwa binadamu.