FAHAMU KUHUSU UGONJWA WA CORONA (COVID-19)
Posted on: April 2nd, 2020Hiki ni kirusi cha aina gani?
Corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kwa wanyama na binadamu. Kwa binadamu, jamii kadhaa za virusi vya Corona vinafahamika kusababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na mfumo wa upumuaji. Maradhi yaliyowahi kusababisha madhara makubwa kutokana na virusi vya Corona ni pamoja na MERS na SARS yaliyozuka mwanzoni mwa miaka ya 2000. Kirusi cha Corona kilichogundulika hivi karibuni kinasababisha ugonjwa unaofahamika kama COVID-19.
COVID-19 ni nini?
COVID-19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Corona. Virusi hivyo vipya havikuwa vikifahamika hapo kabla na sayansi ya tiba. Na vilianzia nchini China mwezi Disemba mwaka 2019.
Dalili za Corona ni zipi?
Dalili kuu za Corona ni pamoja na Homa kali, Uchovu na Kikohozi kikavu na zinatokea taratibu. Dalili kubwa na inayoweza kutia hofu, ni mtu kukosa pumzi. Lakini isikutishe, ni mtu 1 pekee kati ya watu 6 walioambukizwa virusi vya Corona hufikia dalili hiyo ya hatari. Na asilimia 80 ya walio na virusi hivyo hupata nafuu bila kuhitaji msaada wa matibabu.
Makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ni yapi?
WHO inasema wazee na watu wenye magonjwa ya kudumu kama Shinikizo la Damu, Kisukari, Matatizo ya Figo ndiyo walio kwenye hatari zaidi ya kuathika pindi wanapopatwa na virusi vya Corona. Watu wa umri wa wastani na wenye afya imara wanaweza kupata virusi vya Corona na kupona bila kuhitaji matibabu.
Virusi vya Corona vinasambaa vipi?
Watu wanaweza kupata Virusi vya Corona kutoka kwa watu walioambukizwa. Virusi vinaweza kusambaa kupitia maji maji kutoka kwenye pua au mdomo wa aliyeathirika. Iwapo mtu anagusa maji maji kama mafua, mate na makohozi ya mtu aliye na virusi na kisha kujigusa mdomo, macho na pua anaweza kupata virusi vya Corona.
Ninaweza kujikinga vipi na Virusi vya Corona?
- Nawa vizuri na kila wakati mikono yako kwa maji ya vuguvugu, sabuni au dawa za kuua vijijidudu kwa angalau sekunde 20.
- Kaa umbali wa angalau hatua mbili (2) kutoka mtu anayepiga chafya au kukohoa.
- Epuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono hushika sehemu nyingi na ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi.
- Hakikisha wewe, na walio karibu yako wanazingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
- Baki nyumbani ikiwa hujisikii vizuri. Iwapo una mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kwa sababu huko wataalamu watakupatia msaada muhimu
- Epuka kuwa sehemu yenye msongamano, kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye yenye mgandamizo wa hewa.
- Nunua kifunika mdomo na pua na kukikavaa ukiwa kwenye mikusanyiko.
- Fuatilia taarifa za afya na matangazo yake kuhusu virusi vya Corona.
Kwanini watu wanawekwa karantini?
Kwa ufupi neno Karantini linamaanisha kuwa chini ya uangalizi. Watu wenye dalili au wanaotokea maeneo yenye maambukizi makubwa ya virusi vya Corona hulazimikwa kuwekwa karantini (kutengwa na watu wengine) ili kufuatilia afya yao kwa karibu na kuzuia kueneza virusi. Ukiambiwa unapaswa kuwekwa Karantini, usiogope. Ni kwa ajili ya afya yako na wengine.
Virusi vya Corona vina tiba?
Hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya Corona lakini kwa sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba unatumika kupunguza athari za virusi vya Corona.
Ninapaswa kuwa na hofu?
Hapana. Hupaswi kuogopa wala kuwa na hofu. Bali unapaswa kuchukua tahadhari. Kila mtu duniani yuko kwenye uwezekano wa kupata virusi vya Corona lakini kama tulivyokufahamisha, athari zake bado hazitishi.
Ni kweli watu weusi hawawezi kupata Corona?
Hapana, kama ilivyo kwa watu wa rangi na jamii zote sisi watu weusi pia tunaweza kuambukizwa virusi vya Corona. Mfano ni mgonjwa aliyegundulika Kenya.